Jamii ya mchezo nchini Kenya inaomboleza, kufuatia kifo cha ghafla cha mchezaji wa chess Hawi Kaloki.
Chama cha mchezo wa Chess nchini Kenya kimethibitisha kuwa Kaloki alifariki Jumatatu jioni, akiwa na umri wa miaka 19.
Rais wa chama hicho Andrew Owili, alitaja kifo cha Kaloki kuwa pigo kubwa kwa familia yake, marafiki na jamii ya Chess kwa jumla.
Owili alisema taifa hili linamuomboleza sio tu mchezaji shupavu, lakini maisha changa ambayo matumaini yake yamekatwa ghafla.
Kaloki, ndiye mchezaji bora wa Chess nchini Kenya, huku akishinda mataji kadhaa, na alitajwa mchejazi bora nchini Kenya mwaka 2024.
Alikuwa amechaguliwa kuwakilisha Kenya katika michezo ya Chess duniani inayotarajiwa kuanza Tarehe 15 mwezi Septemba 2026.
Aidha, Kaloki alishiriki mashindano ya Chess ya Dunia kwa vijana nchini Brazil 2024 na mashindano ya Chess kwa vijana nchini Albania mwaka 2025. Mashindano ya hivi punde aliyoshiriki akiiwakilisha Kenya ni mashindano ya Chess ya Afrika nchini Botswana.
Kwenye taarifa yake, Owili alituma rambirambi kwa familia ya Kaloki, akisema kuwa familia yake imeomba imwomboleze mpendwa wao faraghani.