Radio Caroline yakosolewa kwa kutangaza kifo bandia cha Mfalme Charles

Jumbe za kumbukumbu ya marehemu zilizorekodiwa mapema zilichezwa hewani kwa bahati mbaya katika kipindi cha Barry Marsh tarehe 19 Mei.

Marion Bosire
2 Min Read

Kituo cha redio cha Caroline huko Uingereza kimekosolewa na shirika la Ofcom baada ya kosa la kushangaza hewani kusababisha kutangazwa kwa taarifa ya uongo kwamba Mfalme Charles III amefariki.

Ujumbe wa kumbukumbu ya marehemu uliorekodiwa mapema ulitangazwa kwa bahati mbaya wakati wa kipindi cha Barry Marsh tarehe 19 Mei, ukidai kwamba Mfalme amefariki na kwamba taarifa hiyo imethibitisha.

Tangazo hilo lilifuatiwa na wimbo wa taifa na dakika 16 za ukimya kwenye DAB+, huku wasikilizaji wa AM wakisikia muziki.

Kituo hicho kilirekebisha tangazo na kuomba msamaha takriban dakika 30 baadaye.

Ofcom iliamua kuwa tukio hilo lilikiuka kanuni za utangazaji zinazotaka habari ziwe sahihi na makosa makubwa yasahihishwe haraka. Ilieleza taarifa hiyo ya uongo kuwa kosa kubwa sana la usahihi kuhusu jambo muhimu sana kwa umma.

Kosa hilo lilitokea mfanyakazi mmoja alipofikia rekodi za taarifa za kifo cha Mfalme Charles zilizotayarishwa kwa ajili ya kutangaza kifo halisi cha Mfalme huyo kitakapojiri.

Mfanyakazi huyo aliripotiwa kuingiwa na hofu baada ya kugundua kosa hilo na kuondoka katika kituo.

Radio Caroline ilisema imechukulia tukio hilo kwa uzito, mfanyakazi huyo alionywa, huku faili hizo zikiondolewa kwenye kompyuta ya studio.

Kituo hicho, kilichoanzishwa mwaka 1964, kinaendelea kurusha matangazo kutoka pwani ya Essex, huku watangazaji wengi wakifanya kazi kwa njia ya mbali.

Share This Article