Seneta wa kaunti ya Nairobi Edwin Sifuna, amesema kuwa kundi la kisiasa la Linda Mwananchi litatumia Katiba kama manifesto yao katika azma ya kumtuma Rais William Ruto nyumbani.
Kiongozi huyo alisema kuwa maendeleo yanaweza kufanywa katika serikali ya kidikteta au ya kidemokrasia.
Akizungumza leo mjini Kitui wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ugavana ya Seneta wa Kitui Enoch Kiio Wambua, Sifuna alisema kuwa ndoto ya upinzani ni kuhakikisha kuwa serikali ijayo inawajibika.
Aliongeza kwamba serikali hiyo, lazima ihakikishie Wakenya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni na kwamba mauaji ya kiholela yanayofanywa nje ya taratibu za kisheria hayatatokea tena nchini.
Alisema kuwa manifesto zote za kisiasa hutokana na Katiba, hivyo Katiba pamoja na kaulimbiu ya “muhula mmoja” vitatumika ipasavyo kumtuma Ruto nyumbani.
Kwa upande wake, Seneta wa Kitui Enoch Kiio Wambua aliahidi kuleta maendeleo makubwa kwa wananchi wa Kitui, akisema kuwa ana uwezo na yuko tayari kutekeleza jukumu hilo.
Wambua alisema pia kwamba kuanzia sasa, ni kusonga mbele daima, hakuna kurudi nyuma katika safari ya kuwania ugavana mpaka mwisho.
Aliwashukuru watu mashuhuri wa Kaunti ya Kitui, kwa kujitokeza kwa wingi pamoja na viongozi wenza kama Sifuna ambao aliahidi kwamba hatawaangusha kwenye uchaguzi wa Agosti 2027.