Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, nchini Tanzania Hamis Mwinjuma,maarufu kama Mwana FA, alihudhuria tamasha ya kusherehekea miaka 30 ya Bongo Fleva.
Hafla hiyo ilifanyika ndani ya ukumbi wa Climax, kwenye jengo la kibiashara la Rock City jijini Mwanza Agosti 8 2026.
Tamasha hiyo iliwakutanisha wanamuziki wakongwe wa Bongo Fleva, ikiwa njia moja ya kuenzi historia, mchango na safari ya muziki huu nchini Tanzania.
Mwinjuma akiwa mgeni rasmi katika tamasha hiyo, alipata pia nafasi ya kuimba pamoja na kundi lake la zamani la East Coast Team. Kundi hilo liliwahi kuwa na wasanii kadhaa akiwemo Crazy GK, AY, Snare na wengine.
Tamasha hiyo imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kukumbusha historia na mchango wa kizazi kilichojenga msingi wa Bongo Fleva nchini Tanzania.