Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan zamu hii amekosa kuongeza muda wa maonyesho ya kimataifa ya kilimo.
Akizungumza jana katika hafla ya kuhitimisha awamu ya mwaka huu ya maonyesho hayo katika uwanja wa Dkt. John Malecela, Nzuguni Jijini Dodoma, Rais Samia alisema wahusika wanahitajika kurejea sehemu zao kuendeleza shughuli za uzalishaji.
“Mwaka jana niliongeza siku mbili, sasa mwaka huu nayafunga leo Jumamosi siongezi siku, kesho Jumapili tufunge virago turudi kwenye maeneo yetu turudi tukazalishe,” alisema Rais Samia.
Katika hafla hiyo Rais Samia aligawa tuzo kwa walioibuka kidedea katika vitengo mbali mbali huku naye akitunukiwa tuzo na Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo, kwa niaba ya Kamati ya Maandalizi ya maonyesho hayo.
Rais Samia Suluhu Hassan alizindua pia magari yatakayotumiwa na Halmashauri ya Taifa ya Huduma za Unyunyiziaji Mashamba Maji, NAESA ambapo alipata fursa ya kuenseha trekta.
Maonyesho hayo ya kimataifa ya Kilimo nchini Tanzania yamepatiwa jina la Nane nane na huanza tarehe Mosi mwezi Agosti kilele kikiwa tarehe nane Agosti kila mwaka.
Yalianzishwa kwa lengo la kukuza uzalishaji na kuhakikisha uendelevu katika kilimo, ufugaji na uvuvi.
Mwaka huu pekee maonyesho hayo yalivutia waonyeshaji bidhaa zaidi ya elfu 1 kutoka ndani na nje ya Tanzania.