KWS yaimarisha uchunguzi wa vifo vya ndovu 16 Amboseli

Kulingana na shirika hilo la KWS, vifo vya ndovu hao vilitokea kati ya 24 Juni na 31 Julai 2026.

Tom Mathinji
2 Min Read
KWS yaimarisha uchunguzi dhidi ya ndovu 16 Amboseli.

Shirika la Huduma kwa Wanyama Pori (KWS), limeanza uchunguzi wa kina kuhusu kufariki kwa ndovu 16 kwenye mfumo ikolojia wa Amboseli – Kimana – Kitenden.

Kulingana na shirika hilo la KWS, vifo vya ndovu hao vilitokea kati ya 24 Juni na 31 Julai 2026.

“KWS imepeleka kundi la madaktari na wanasayansi kutoka Nairobi, Tsavo na Amboseli, kuwatibu wanyama walioathirika, kutekeleza uchunguzi wa maiti, kukusanya sampuli na kuimarisha uchunguzi,” lilisemashirika hilo kupitia taarifa kwenye ukurasa wa X.

Kwenye taarifa hiyo, KWS ilisema inashirikiana kwa karibu na serikali pamoja na Chuo Kikuu cha Nairobi, kufanyia uchunguzi wa maabara sampuli zilizokusanywa kutoka kwa ndovu waliofariki.

Aidha, shirika hilo lilidokeza kuwa uchunguzi wa awali uliotekelezwa na Chuo kikuu cha Nairobi, uliashiria kuwa huenda vifo hivyo vilisababishwa na sumu aina ya Cyanide.

“Uchunguzi zaidi wa kimaabara kuthibitisha matokeo hayo unaendelea, ili kubaini kiini halisi cha kifo cha kila ndovu na kubaini chanzo halisi cha sumu hiyo,” iliongeza shirika hilo.

KWS ilidokeza kuwa imeiomba Bodi ya Kudhibiti Dawa za Kuangamiza Wadudu kutekeleza uchunguzi kubaini iwapo dawa za kuwaangamiza wadudu au kemikali zingine huenda zilitumika vibaya, kuhifadhiwa au kutupwa katika mfumo mpana ikolojia wa Amboseli.

Wakati huo huo KWS imesema inatekeleza doria za uangalizi wa ndovu katika eneo hilo, huku ikitoa ahadi ya kutangaza matokeo ya uchunguzi wake punde tu utakapokamilika.

TAGGED:
Share This Article