Mateka zaidi ya 300 waokolewa nchini Nigeria

Waathiriwa hao waliokolewa kutoka mbuga ya kitaifa ya Kainji katika jimbo la Niger kwenye oparesheni iliyohusisha jeshi,polisi na maafisa wa ujasusi.

Tom Mathinji
1 Min Read
Bola Tinubu - Rais wa Nigeria.

Vikosi vya Usalama nchini Nigeria, vimefanikiwa kuwaokoa mateka zaidi ya 300,katika kile kimetajwa kuwa operesheni kubwa zaidi ya siku moja katka historia ya taifa hilo.

Waathiriwa hao waliokolewa kutoka mbuga ya kitaifa ya Kainji katika jimbo la Niger kwenye oparesheni iliyohusisha jeshi,polisi na maafisa wa ujasusi.

Miongoni mwa waliokolewa ni watu 163 walioshikwa mateka mwezi Februari mwaka huu kwenye uvamizi wa jimbo la Kwara,na 145 kutoka jimbo la Niger, ambapo watu kadhaa waliuawa.

Msemaji wa afisi ya Rais Bayo Onanuga, amesema msako huo ndio mkubwa zaidi kuwahi kutekelezwa kwa siku moja.

Maafisa nchini humo wanasema waathiriwa hao kwa sasa wanapokea matibabu katika kituo kimoja cha kijeshi, kabla ya kuunganishwa tena na familia zao.

Rais wa Nigeria Bola Tinubu alisema kupitia kwa taarifa kwamba ufanisi wa operesheni hiyo ya kijasusi, inaashiria ukuaji wa ushirikiano miongoni mwa asasi za usalama za taifa hilo.

“Nawapongeza maafisa wetu wa usalama kwa ujasiri wao na kujitolea kulinda maisha ya raia wa Nigeria,” alisema Tinubu.

Kulingana na msemaji wa serikali Bayo Onanuga, operesheni hiyo ya uokoaji ni sehemu ya juhudi ya Rais Tinubu za kudumisha amani katika sehemu zote za taifa hilo.

Share This Article