Bunduki 2,000, risasi 15,000 zimetwaliwa kutoka kwa wahalifu, asema Murkomen

Murkomen alipongeza Huduma ya Taifa ya Ujasusi (NIS) na Huduma ya Taifa ya Polisi (NPS), kwa ufanisi huo.

Tom Mathinji
2 Min Read
Bunduki 2,000 na risasi 15,000 zimetwaliwa kutoka kwa wahalifu.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amepongeza Kikosi cha Maafisa wa Usalama cha Special Operations Group (SOG), akisema kimefanikiwa kukabilina na ujangili na ugaidi katika Bonde la Kerio na sehemu zingine za nchi.

“Zaidi bunduki 2,000 na risasi 15,000 zimetwaliwa kutoka mikononi mwa majangili na magaidi,” alisema Murkomen.

Aliyasema hayo Alhamisi alipoongoza sherehe za 11 za kufuzu kwa kikosi hicho cha SOG, katika chuo cha mafunzo cha Kamanga kaunti ya Samburu.

Waziri huyo aliwapongeza maafisa 122 kwa kukamilisha mazoezi ya miezi sita na nusu, akiwahimiza kuwahudumia Wakenya kwa utaalam na Maadili ya hali ya juu, akitaja jukumu muhimu ambalo hutekelezwa na kikosi hicho kwa kuhakikisha usalama hapa nchini.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, aongoza sherehe ya 11 ya kufuzu kwa maafisa wa usalama wa kikosi cha SOG kaunti ya Samburu.

“Mmeitwa kukabiliana na ghasia, kusambaratisha mitandao ya wahalifu, kuangamiza hatari mipakani, kulinda miundombinu ya taifa na kupiga jeki operesheni maalum, ambapo nidhamu na utaalam ni muhimu zaidi,” alisema Murkomen.

Wakati huo huo, Waziri huyo alipongeza Huduma ya Taifa ya Ujasusi (NIS) na Huduma ya Taifa ya Polisi (NPS), kwa ufanisi huo, akielezea lengo la serikali la kufanya mabadiliko katika sekta ya usalama ili iwe bora zaidi.

Kwenye sherehe hiyo Murkomen alikuwa ameandamana na Mkurugenzi Mkuu wa NIS Noordin Ali, Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli, na maafisa wengine wa usalama wa ngazi za juu.

Share This Article