Wembly Mo alivyowezesha Ghetto Kids kufika Marekani

Alitoa gari lake binafsi liuzwe ili kundi hilo lipate fedha za safari, licha ya yeye kutosafiri nao.

Marion Bosire
2 Min Read

Meneja wa kundi maarufu la densi la watoto nchini Uganda ‘Triplets Ghetto Kids’, Dauda Kavuma, amefichua kujitolea kwa kipekee kulikofanywa na mcheza densi Wembly Mo.

Jambo hilo liliwezesha kundi hilo kutumbuiza kwenye onyesho kubwa la wakati wa mapumziko ya fainali ya Kombe la Dunia la FIFA nchini Marekani pamoja na nyota wa kimataifa wa muziki Shakira na Burna Boy.

Akizungumza baada ya kundi hilo kurejea Uganda, Kavuma alisema walikumbana na changamoto ya kupata fedha za kulipia tiketi za ndege licha ya kupokea mwaliko huo wa heshima.

Hakuwa na uhakika wa namna ya kupata fedha hizo akalazimika kumfuata Wembly Mo kuomba msaada.

Ingawa Mo hakuwa na fedha taslimu, alijitolea kutoa gari lake binafsi liuzwe ili kundi hilo lipate fedha za safari, licha ya yeye kutosafiri nao.

Kavuma alieleza kitendo hicho kuwa ni cha kujitolea kwa dhati na kusema kinaonyesha moyo wa Wembly Mo wa kuwasaidia wengine bila kutarajia malipo.

Aliongeza kuwa msanii huyo amekuwa akibadilisha maisha ya watu wengi kimya kimya kwa miaka mingi bila kupata kutambuliwa anavyostahili.

Kavuma alisema aliamua kuweka hadharani mchango huo kwa sababu ulikuwa sababu muhimu iliyowawezesha Ghetto Kids kutumia fursa hiyo ya kipekee maishani.

Kundi hilo linaendelea kuitangaza Uganda kupitia maonyesho yake katika majukwaa makubwa ya kimataifa duniani.

Wembly Mo ambaye jina ake halisi ni Moses Kyeyune ni mcheza densi , mbunifu wa miondoko ya densi, jaji wa mashindano ya densi na mhisani mashuhuri kutoka Uganda, anayeishi Kampala.

Anajulikana sana kama mwanzilishi wa wakfu wa Wembly Mo, taasisi ya hisani inayotumia densi na sanaa kama njia ya kuwaokoa, kuwalea, kuwapa mwongozo, na kubadilisha maisha ya watoto walio katika mazingira magumu na wanaoishi mitaani nchini Uganda.

Share This Article