Museveni ahimiza kurahisishwa kwa masharti ya ndoa

Ameonya kuwa kugeuza ndoa kuwa biashara kunawakatisha tamaa vijana kuanzisha familia

Marion Bosire
1 Min Read
Rais wa Uganda Yoweri Museveni.

Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni amehimiza jamii yake ya Banyankole kurahisisha masharti ya ndoa.

Kiongozi huyo anasema jamii hiyo inastahili kuacha kudai mahari ya kiwango cha juu na kufanya sherehe za harusi za gharama kubwa, akionya kuwa kugeuza ndoa kuwa biashara kunawakatisha tamaa vijana kuanzisha familia.

Akizungumza Jumamosi katika sherehe ya mahari ya Kisha Isabel Byanjeru Kaboyo, binti wa Waziri wa Nchi wa Luweero Triangle na Rwenzori, Alice Kaboyo, Museveni alisema kudai fedha nyingi na mifugo kama mahari kumeifanya ndoa kuwa mzigo wa kifedha.

Alihoji ni kwa nini baadhi ya familia zinadai hadi ng’ombe 15 na mamilioni ya pesa, hali inayowalazimu vijana wengi kuanza maisha ya ndoa wakiwa na madeni.

Rais huyo alikosoa pia harusi za kifahari, akisema zinaziwekea familia mzigo usio wa lazima wa matumizi makubwa.

Alitoa mfano wa ndoa yake na Mama wa Taifa Janet Museveni, akisema walifanya sherehe rahisi nje ya nchi iliyohudhuriwa na wageni wanane pekee.

Museveni aliwataka viongozi wa kijamii na wa dini kuhimiza ndoa nafuu ili kuhifadhi umuhimu wa kitamaduni wa sherehe ya Okuhingira na wakati huo huo kufanya ndoa iwe nafuu na rahisi zaidi kwa vijana nchini.

 

Share This Article