Mama Dangote avunja kimya, akaribisha mjukuu

Alichapisha picha moja ya Diamond, Zuchu na mwanao katika chumba cha hospitali na kuandika maneno ya kumkaribisha.

Marion Bosire
1 Min Read

Mamake mwanamuziki wa Tanzania Diamond Platnumz ambaye hujirejelea kama Mama Dangote kwenye Instagram hatimaye amevunja kimya chake na kukaribisha mjukuu wake.

Mama huyo ambaye jina lake halisi ni Sanura Kassim alichapisha ile picha moja ya Diamond, Zuchu na mwanao katika chumba cha hospitali na kuandika maneno ya kumkaribisha.

“Karibu Bi Mdogo wangu (N) Bint Naseeb Kichwa!! Tunakupenda Sana,” aliandika mama huyo huku akiendelea kumtania dogo huyo kwamba akue ili achukue mume wake na arithi shingo yake.

Chini ya chapisho hilo Zuchu aliandika, “Asante bibi ake mjukuu”, ujumbe aliomalizia na kopa ishara ya mapenzi.

Bi. Sanura amekuwa kimya kuhusu suala zima la mahusiano ya Diamond na Zuchu tangu awali isipokuwa video moja ya mahojiano ambapo anaonekana kujibu mwanahabari akisema yeye anafahamu kwamba Zuchu ni msanii tu wa Diamond Platnumz.

Aliposherehekea siku yake ya kuzaliwa, Zuchu hakuwepo wengi wakikisia kwamba ni kwa sababu hawana uhusiano mwema lakini mwandani wa Diamond, Baba Levo aliambia wanahabari kwamba Zuchu alikuwa mjamzito na hangeweza kuhudhuria.

Mama Sanura hakuhudhuria sherehe ya Zuchu ya kukaribisha mwanawe ambayo Diamond Platnumz alifika akiwa amechelewa.

Share This Article