Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki, yuko nchini Uganda kuhudhuria kongamano la pili la Afrika kuhusu kikosi cha kuleta Udhabiti na Utulivu nchini Somalia (AUSSOM).
Kindiki anahudhuria kongamano hilo kwa niaba ya Rais William Ruto, huku viongozi wa kikanda wakikadiria juhudi za kuimarisha usalama na utulivu katika taifa hilo la upembe wa Afrika.
“Nimewasili Jijini Entebbe, Uganda kuwakilisha Kenya katika kongamano la pili lisilo la kawaida la Umoja wa Afrika kuhusu Udhabiti nchini Somalia (AUSSOM), kwa niaba ya Rais William Ruto,” alisema Kindiki kwenye ukurasa wa X.
Mkutano huo wa siku mbili unawaleta pamoja Marais na Maafisa Wakuu wa serikali kutoka Burundi, Djibouti, Misri, Ethiopia, Kenya, Somalia na Uganda, pamoja na wawakilishi wa ngazi ya juu kutoka Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa (UN) na shirika la maendeleo la IGAD.
Kikosi cha ‘AUSSOM’ kimejukumiwa kukabiliana na kundi la kigaidi la Al-Shabaab, kuwalinda raia, na kuhakikisha mazingira bora kwa uhamisho wa majukumu ya kiusalama kwa vikosi vya usalama nchini Somalia.