Maandamano yazuka Tripoli, Libya kulalamikia kukatika kwa umeme

Wengi wao wakiwa vijana, waandamanaji walifunga ofisi za kampuni ya mawasiliano ya serikali ya Libya na wilaya ya Souq Al-Jumaa

Marion Bosire
2 Min Read

Maandamano ya kulalamikia kukatika kwa umeme yamezuka jijini Tripoli nchini Libya ambapo Waandamanaji wamefunga barabara na Wizara ya Mambo ya Nje jijini Tripoli.

Wanaendeleza kampeni ya kutotii mamlaka, iliyoanzishwa kupinga kukatika kwa umeme na gharama kubwa za huduma ya umeme na ambayo imeenea katika maeneo zaidi.

Makundi ya watu yaliziba barabara ya pwani katika eneo la Janzour, magharibi mwa Tripoli, siku ya Jumapili, na kukusanyika nje ya kituo cha kuzalisha umeme cha West Tripoli wakipinga kukatika kwa umeme kwa saa nyingi.

Video zilizochapishwa mtandaoni zinaonyesha waandamanaji wakichoma matairi hadi alfajiri ya Jumatatu na kufunga barabara kuu katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu.

Picha hizo pia zinaonyesha waandamanaji wakimwaga udongo kutoka kwenye lori mbele ya Wizara ya Mambo ya Nje mjini Tripoli katika jaribio la kuifunga.

Wengi wao wakiwa vijana, waandamanaji hao pia walifunga ofisi za kampuni ya mawasiliano ya serikali ya Libya na wilaya ya Souq Al-Jumaa, kwa mujibu wa chombo cha habari cha Libya Review, huku wakibeba mabango yanayomkosoa Waziri Mkuu Abdul Hamid Dbeibah.

Kampeni hiyo ilianzishwa na Harakati ya Souq Al-Jumaa, ambayo imekuwa ikiipinga Serikali ya Umoja wa Kitaifa tangu Mei 2025. Katika taarifa yake ya Jumapili, harakati hiyo ilisema lengo lake ni “kuipooza kabisa serikali” badala ya kuvuruga maisha ya kawaida ya wananchi.

Pia ilitaka uwajibikaji kuhusu madai ya ufisadi na kuvunjwa kwa taasisi za kisiasa zilizopo nchini Libya, zikiwemo serikali, Baraza la Wawakilishi, Baraza la Taifa na Baraza la Rais.

Share This Article