Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa Meru kukutana Jumamosi

Rais William Ruto anatarajiwa kuongoza hafla hiyo.

Marion Bosire
2 Min Read
Rais William Ruto

Maandalizi ya maadhimisho ya Jumamosi Julai 25, 2026 ya siku ya wafugaji wa ng’ombe wa maziwa Meru, yamekamilika kwa kiwango kikubwa huku Rais William Ruto akitarajiwa kuongoza.

Waandalizi wamekamilisha shughuli ya kuweka mahema, viti, skrini kubwa na miundombinu mingine muhimu katika Uwanja wa Maonyesho wa ASK Meru kwa ajili ya hafla hiyo inayotarajiwa kuhudhuriwa na wafugaji elfu 45, kutoka maeneo mbalimbali ya ukanda huo.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maandalizi katika uwanja huo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Muungano wa Ushirika wa Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa wa Meru, Kenneth Gitonga, alisema siku hiyo itawezesha wafugaji kujifunza teknolojia za kisasa za ufugaji, mbinu bora za utunzaji wa mifugo na ubunifu wa kuongeza uzalishaji wa maziwa.

Gitonga alisema kwa sasa muungano huo hukusanya takriban lita 670,000 za maziwa kila siku na unalenga kufikia lita milioni moja kupitia mbinu bora za ufugaji.

Aliongeza kuwa Rais Ruto atazindua rasmi kiwanda cha kutengeneza chakula cha mifugo cha muungano huo kinachotarajiwa kupunguza gharama za chakula cha mifugo na kuongeza mapato ya wafugaji.

Wahudhuriaji wataangazia udhibiti wa magonjwa ya mifugo, matumizi ya teknolojia nafuu za uzalishaji wa mifugo, mfumo wa malipo ya maziwa kulingana na ubora wake na kupanua masoko ya nje.

Mwenyekiti wa Muungano huo, Simon Kiruja, aliwahimiza vijana kujitosa katika ufugaji wa maziwa, akisema ni sekta yenye faida na endelevu kwa ukuaji wa uchumi wa baadaye.

Share This Article