Rais William Ruto amemteua Samuel Muchina Nyaga, aliyekuwa mgombea wa chama cha UDA, katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol Kalou uliomalizika hivi maajuzi, kuwa mjumbe wa Tume ya Mito ya Nairobi.
Kupitia Notisi ya Gazeti Rasmi la Serikali iliyochapishwa Julai 22, 2026, Rais Ruto alitangaza uteuzi wa Muchina na wakati huohuo akabatilisha uteuzi wa Amos Chege Mugo, ambaye alikuwa akihudumu kama mjumbe wa Tume ya Mito ya Nairobi.
“Mimi, William Samoei Ruto, Rais wa Jamhuri ya Kenya na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, namteua Samuel Muchina Nyaga kuwa Mjumbe wa Tume ya Mito ya Nairobi kuanzia tarehe 22 Julai, 2026,” ilisema sehemu ya notisi hiyo.
Kiti cha ubunge cha Ol Kalou kilibaki wazi baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo, Njuguna Kiaraho.
Tume ya Mito ya Nairobi ilianzishwa kusimamia ukarabati, urejeshaji na ulinzi wa mito ya Nairobi pamoja na mifumo yake ya ikolojia, kwa lengo la kuboresha mazingira na kuhifadhi rasilimali za maji katika jiji hilo.