Idara ya mahakama ya Kenya imesisitiza tena msimamo wake wa kutovumilia rushwa kufuatia kukamatwa kwa Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama ya Kangema, Martin Kinyua Mutegi.
Alikamatwa pamoja na afisa wa huduma za uangalizi kwa tuhuma za kuomba na kupokea hongo kuhusiana na kesi iliyokuwa ikiendelea mahakamani.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, Jaji Mkuu na Rais wa Mahakama ya Juu, Martha Koome, alisema tuhuma hizo ni nzito na kwamba zikithibitishwa, zinadhoofisha imani ya umma katika utoaji wa haki.
Alisisitiza kuwa maafisa wa mahakama wanapaswa kuzingatia viwango vya juu vya uadilifu, uwajibikaji, uwazi na kutopendelea upande wowote, akiongeza kuwa waliopatiwa jukumu la kusimamia haki hawawezi kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Jaji Mkuu alitangaza kuwa Idara ya Mahakama na Tume ya Huduma za Mahakama zimeanzisha taratibu za kinidhamu na kiutawala dhidi ya hakimu huyo kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Huduma za Mahakama na sera husika za rasilimali watu.
Akisubiri kukamilika kwa mchakato huo, ameondolewa kwa muda katika majukumu yake ya mahakama ili asiathiri uchunguzi wa jinai unaoendelea.
Koome alisema Mahakama itashirikiana kikamilifu na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC na mashirika mengine ya uchunguzi ili kuhakikisha sheria inafuatwa.
Alihakikishia Wakenya kuwa hatua madhubuti zitachukuliwa dhidi ya afisa yeyote wa mahakama au mfanyakazi atakayebainika kukiuka maadili na sheria.