Navio asema ushirikiano na bendi ya Afrigo ulimjaza hisia

Anasema alikaribia kulia akiwa studio na wanachama wa bendi hiyo na mwanzilishi Moses Matovu

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa mtindo wa Rap nchini Uganda Navio amezungumzia ushirikiano wake na bendi ya Afrigo katika kurekodi albamu yake ijayo, akisema ulimjaza hisia.

Msanii huyo ambaye jina lake halisi ni Daniel Kigozi Lubwama, alifichua kuwa alikaribia kulia akiwa studio na wanachama wa bendi ya Afrigo pamoja na mwanamuziki mkongwe Moses Matovu.

Alikuwa akizungumza kwenye mahojiano ambapo alitambua mchango wa watu mbalimbali waliokuwa na ushawishi mkubwa katika tasnia ya muziki nchini Uganda, kabla na baada ya kizazi chake lakini akasisitiza kuhusu Moses Matovu.

Navio alimsifu Matovu kwa kudumu kwa muda mrefu katika tasnia ya muziki, akibainisha kuwa mwanzilishi huyo wa Afrigo Band ameburudisha mashabiki kwa miaka 52.

Rapa huyo aliendelea kueleza kuwa ushirikiano huo ulihusisha wimbo maarufu wa Afrigo uitwao “Sikulimba”, ambao, kwa mujibu wake, ulikuwa haujaguswa kwa zaidi ya miongo minne.

“Hakuna aliyegusa ‘Sikulimba’ kwa takribani miaka 40 hadi 46. Hawakumruhusu mtu yeyote kuufanyia kazi. Hivyo, Matovu alipokuja studio, aliusikiliza, akauvutiwa nao na akaamua kushiriki kuucheza. Ulikuwa ushirikiano wa moja kwa moja.” Alisema.

Navio alikiri kuwa uzoefu huo ulimzidia hisia kwa sababu kwa muda mrefu amekuwa mmoja wa mashabiki wakubwa wa mwanamuziki huyo mkongwe.

Mbali na muziki, Navio alisema pia alivutiwa na nguvu, nidhamu na mtindo wa maisha wa Matovu, akimtaja kuwa mwenye afya nzuri na mwenye hekima nyingi.

 

Share This Article