Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, amesema Kenya inaunga mkono kikamilifu mchakato wa kuleta amani nchini Sudan.
Akizungumza kwenye mkutano wa tatu wa IGAD uliowaleta pamoja wajumbe maalum na wawakilishi wa mchakato wa amani wa Sudan, Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, alisema Kenya inaendelea kujitolea kubuni fursa zitazoleta suluhu za kudumu kupitia majadiliano wala sio mizozo.
“Kenya pia inakaribisha juhudi zinazoendelea za kimataifa ikiwa ni pamoja na mkataba wa Jeddah na mkakati wa Quad, huku ikunga mkono maamuzi ya Umoja wa Afrika, IGAD , na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kusuluhisha mzozo nchini Sudan,” alisema Mudavadi.
Kulingana na Mudavadi, jukumu la pamoja ni kuimarisha mchakato wa mapatano unaoongozwa na Afrika, na kuhakikisha ushirikiano wa karibu na jamii pana ya kimataifa.
“Kwa kuleta amani Sudan, tunalinda uthabiti wa kikanda, kupanua fursa za biashara na uwekezaji, kuimarisha usalama wa mipakani na kuboresha uchumi wa Afrika Mashariki,” aliongeza waziri huyo.
Alisema Kenya itaendelea kutekeleza jukumu lake kama mshirika wa kuaminika, ili kufanikisha ajenda ya amani na usalama Afrika, kwa manufaa ya kanda hii na raia wake.