Kesi inayochunguza mauaji ya mwalimu na mwanablogu Albert Ojwang, inaingia siku ya tatu leo Jumatano katika Mahakama Kuu ya Kibera.
Awali Justice Diana Kavedza aliwauliza mawakili wanaohusika na kesi hiyo ikiwa watajiunga na wenzao wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) ambao wamepanga kususia vikao vya mahakama leo Jumatano, lakini walisema wako tayari kuedelea na kesi hiyo jinsi ilivyopangwa.
Mtaalamu wa kisayansi wa Halmashauri ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA), aliyeanza kuwasilisha ushahidi Jumanne alasiri, anatarajiwa kuendelea kutoa ushahidi Jumatano, kabla ya mashahidi wengine wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wao.
Justice Kavedza, alielezea nia yake ya kukamilisha kesi hiyo katika muda wa miezi sita.
Alizitaka pande husika kuwa tayari kuhudhuria vikao hivyo kulingana na tarehe zilizotengwa, kwa lengo la kuharakisha utekelezaji wa haki.
Aliyekuwa Afisa Mkuu wa kituo cha Polisi cha Central Jijini Nairobi (OCS) Samson Talaam, Konstebo wa Polisi Peter Kimani, mwenzake James Mukhwana, na raia wengine watatu ambao wameshtakiwa kwa mauaji hayo, wamekanusha mashtaka dhidi yao.