Wadau wahimizwa kuwekeza katika ubunifu

Wito huu ulitolewa katika hafla ya kufunga awamu ya 12 ya tamasha ya sanaa ya Ubumuntu, jijini Kigali, nchini Rwanda.

Marion Bosire
2 Min Read
Sandrine Umutoni, Waziri wa vijana na sanaa nchini Rwanda.

Awamu ya 12 ya tamasha ya sanaa ya Ubumuntu ilifika kikomo Jumapili kwa wito mpya kwa wadau kuwekeza katika sekta ya ubunifu kama chombo cha kuleta uponyaji, kujenga amani na kuchochea maendeleo ya taifa.

Akizungumza katika hafla ya kufunga tamasha hiyo katika kituo cha kumbukumbu ya mauaji ya halaiki jijini Kigali, Waziri wa vijana na sanaa, Sandrine Umutoni, aliwahimiza Wanyarwanda kuiona sanaa kuwa zaidi ya burudani.

Alisema kuwa ubunifu una nafasi muhimu katika kuhifadhi kumbukumbu za historia, kuimarisha jamii na kujenga mustakabali wa nchi.

Waziri huyo alisisitiza tena dhamira ya serikali ya kukuza uchumi wa ubunifu kupitia uwekezaji unaozalisha ajira, kuwaunga mkono wasanii na kuitangaza hadithi ya Rwanda duniani.

Mwanzilishi wa tamasha hiyo, Hope Azeda, alisema kuwa awamu ya mwaka huu ilivutia washiriki kutoka zaidi ya nchi 15 licha ya changamoto za kimataifa, kama mlipuko wa Ebola.

Azeda alizungumzia kuanzishwa kwa mpango wa afya ya akili chini ya kaulimbiu “Nani Anamponya Mponyaji?” akiutaja kuwa hatua muhimu, akisisitiza umuhimu wa kusaidia wasanii wanaokabiliwa na msongo wa mawazo, uchovu wa kazi na changamoto nyingine za afya ya akili.

Waandaaji pia walizindua mpango wa Ubumuntu Green Circle, unaowahamasisha wabunifu kutanguliza afya yao ya akili, na kutangaza mpango wa kuanzisha Cave of Hope, kituo cha kudumu cha sanaa kitakachokuwa na kumbi za mazoezi, sehemu za maonyesho na malazi kwa wasanii.

Share This Article