Rais William Ruto ameusifia ushirikiano uliopo kati ya Kenya na Umoja wa Ulaya (EU) akiutaja umoja huo kuwa mshirika wa kimkakati wa pande mbili wa nchi hii.
Hususan, amesema uhusiano huo wa muda mrefu ulipigwa jeki kupitia kusainiwa kwa Makubaliano ya Ushirikiano wa Ulaya (EPA) mwezi Julai mwaka 2024.
“EPA inatoa fursa kwa bidhaa za Kenya ikiwa ni pamoja na maua, majani chai, na kahawa kuuzwa katika soko la Ulaya bila kutozwa ushuru. Kwa uapnde wake, EU inauza humu nchini mashine, kemikali na bidhaa za madini,” alisema Rais Ruto.
“Tangu kusainiwa kwa EPA, biashara yetu imeongezeka kwa asilimia 20, na kufanya biashara yetu ya kila mwaka kufikia dola bilioni 3.8 sawa na shilingi bilioni 494 za Kenya.”
Rais aliyasema hayo katika Ikulu ya Nairobi alipomwaga Balozi wa EU humu nchini Henriette Geiger.
Alimsifia Balozi huyo akisema kwa kipindi alichohudumu, uhusiano kati ya pande hizo mbili uliimarika kwa kiwango kikubwa.
Ushirikiano kati ya pande hizo unaangazia nyanja kama vile uvumbuzi wa kidigitali, mabadiliko ya tabia nchi na usalama wa kikanda.