Ruto azindua mashauriano na maandalizi ya ripoti kuhusu uwazi

Ripoti hiyo, inayotarajiwa kuzinduliwa baadaye mwaka huu, itakuwa ya kwanza ya aina yake duniani.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amezindua mashauriano yatakayowezesha maandalizi ya ripoti ya kwanza ya hali ya uwazi nchini Kenya.

Kiongozi wa nchi alielezea hatua hiyo kuwa muhimu katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na kuendeleza imani ya wananchi kwa serikali.

Akizungumza katika Ikulu, Nairobi jana, Rais Ruto alisema ripoti hiyo itaweka kiwango cha kitaifa cha kupima uwazi, utendaji wa taasisi na uwajibikaji katika serikali, huku ikibainisha maeneo yanayohitaji kuboreshwa ili kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi.

Rais alisema serikali inaendelea kuimarisha uwazi kwa kupanua upatikanaji wa taarifa kwa umma katika wizara, idara na mashirika ya serikali.

Alibainisha kuwa idadi ya huduma za serikali zilizowekwa kwenye mfumo wa kidijitali imeongezeka kutoka huduma 350 mwaka 2022 hadi zaidi ya huduma 26,000, hatua iliyoboresha ufanisi, upatikanaji wa huduma na uwajibikaji.

Rais Ruto pia alielezea mageuzi mbalimbali yaliyotekelezwa, kama Mfumo Jumuishi wa Malipo ya Kidijitali wa Serikali ili kudhibiti uvujaji wa mapato, mfumo wa ununuzi wa kielektroniki ili kuimarisha uwazi katika matumizi ya fedha za umma, ajira za ushindani na zenye kuzingatia sifa katika mashirika ya umma, pamoja na Sheria ya Migongano ya Maslahi iliyopitishwa hivi karibuni ili kuimarisha uadilifu katika uongozi wa umma.

Alisema hatua za kuimarisha uwazi pia zimejumuishwa katika utekelezaji wa Mfuko wa sheria ya hazina ya kitaifa ya miundombinu kupitia mageuzi yanayolenga kuimarisha uhuru wa taasisi na uwajibikaji.

Rais aliagiza wizara zote, idara, mashirika ya serikali, tume za kikatiba na serikali za kaunti kushirikiana kikamilifu na Tume ya Haki za Kiutawala katika zoezi hilo kwa kutoa taarifa sahihi, kamili na kwa wakati.

Aliongeza kuwa ripoti hiyo, inayotarajiwa kuzinduliwa baadaye mwaka huu, itakuwa ya kwanza ya aina yake duniani.

Share This Article