Argentina yafuzu fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya pili mtawalia

Argentina watashuka uwanjani New York, New Jersey Jumapili, Julai 19 usiku kwa fainali dhidi ya mabingwa wa mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.

Dismas Otuke
2 Min Read

Argentina ilihitaji dakika saba Jumatano usiku kufunga mabao 2 na kuwalaza Uingereza 2-1 na kujikatia tiketi kwa fainali ya Kombe la Dunia kwenye mechi iliyosakatwa uwanjani Atlanta, Marekani.

Baada ya timu zote kutoshana nguvu katika kipindi cha kwanza, Uingereza maarufu kama Three Lions walirejea kwa matao ya juu na ushirikiano bora kati ya Morgan Rodgers na Antony Gordon, ulimpa Gordon fursa ya kupachika bao la kwanza dakika ya 55.

Hata hivyo, Waingereza walihiari kujihami huku pia kocha wao akifanya mabadiliko mabovu ya wachezaji akilenga kulinda uongozi huo wa goli moja.

Zikisalia dakika tano mechi ikamlike, Enzo Fernandez alifyatua tobwe lililotuama kimiani  baada ya kuungisha pasi yake Lionel Messi na kuwapa Argentina ukipenda La Albiceleste, bao la kusawazisha.

Uingereza wakisubiri mechi ielekee muda wa ziada wa dakika 30, walipigwa na butwaa baada ya nguvu mpya wa Argentina Lautaro Martinez kutikiza wavu kwa kichwa kwa bao la ushindi katika dakika ya 92, kufuatia pasi murua yake Messi.

Mwisho wa siku, zilikuwa hisia mseto uwanjani, Argentina wakilia machozi ya furaha ya kupata ushindi ambao unawapeleka fainali wakiwinda kombe la tatu, nao Uingereza wakilia kwa kukosa kufuzu kwa fainali baada ya subira ya miaka 60.

Argentina watashuka uwanjani New York, New Jersey Jumapili Julai 19 usiku, kwa fainali dhidi ya mabingwa wa mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.

Kabla ya hapo, Uingereza watakumbana na Ufaransa kuwania nishani ya shaba Jumamosi, usiku wa manane.

Share This Article