Rais wa Marekani Donald Trump amesema ameachana na mpango wake wa kutoza ushuru katika Mlango Bahari wa Hormuz.
Awali, Trump alitangaza kuwa atatoza ushuru wa asilimia 20 kwa meli zinazopitia katika mlango bahari huo.
Hata hivyo, amesema ameachana na mpango huo baada ya kupigiwa simu na viongozi wa nchi mbalimbali wakielezea mashaka kutokana na mpango huo.
Ameongeza kuwa hatua yake imetokana na ukweli kwamba viongozi wa mataifa ya eneo la Mashariki ya Kati wameelezea dhamira ya kuwekeza nchini Marekani.
“Saudi Arabia, UAE, Qatar, Bahrain na Kuwait, unafahamu, kimsingi, na kisha zinginezo. Nilizungumza nao wote na wangependa kuwekeza nchini Marekani kiasi kikubwa cha fedha zaidi kuwahi kushuhudiwa. Kwa misingi hiyo, sitatoza ushuru. Sipendi dhana ya ushuru,” alisema Trump wakati akiwahutubia wanahabari.
Rais huyo wa Marekani ameendelea kuiwekea Iran shinikizo la kijeshi huku Kamandi Kuu ya nchi hiyo, CENTCOM ikianza tena kuzuia meli zinazosafiri kwenda au kutoka bandari za Iran na maeneo ya pwani.