Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa makubaliano kati ya Marekani na Iran “yameingia katika mgogoro.”
Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vinamnukuu Esmail Baghaei akisema kwamba “mashambulizi ya kujihami” ya Iran yamelenga tu kambi na vituo vilivyotumiwa na Marekani kushambulia nchi hiyo.
“Hatutasita kujilinda,” ameongeza, akisema kuwa Iran haiwezi kuruhusu Marekani kutumia njia ya usafiri kupitia Mlango wa Bahari wa Hormuz kuhatarisha mamlaka na usalama wa nchi hiyo.
Baghaei amesema kuwa mazungumzo ya Jumamosi yalihusu tu njia hiyo muhimu ya baharini, akiongeza kuwa lengo la Iran lilikuwa kuhakikisha meli zinapita kwa usalama. Hata hivyo, amesema kuwa shinikizo la Marekani kwa Oman limekwamisha juhudi hizo.
Kwa ukumbusho, takwimu za ufuatiliaji wa meli zinaonesha kuwa hakuna meli iliyopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz tangu jana jioni.
Kuhusu Hati ya makubaliano yenye vipengele 14 yaliyotiwa saini tarehe 17 Juni, Baghaei amesema kuwa Iran haitatekeleza wajibu wake ikiwa Marekani haitaheshimu makubaliano hayo.
Taarifa ya BBC