Jude Bellingham alipachika magoli mawili na kuisaidia Uingereza kujikatia tiketi kwa nusu fainali ya Kombe la Dunia, kufuatia ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya Norway, Jumamosi usiku katika uchanjaa wa Miami.
Andreas Schjelderup alikuwa amemaweka Norway uongozini dakika 36, naye Bellingham, akakomboa goli hilo na kipindi cha kwanza kuishia sare ya 1-1.
Pande zote zilicheza mchezo wa kuviziana kipindi cha pili lakini milango yote ilikuwa imara na kulazimu Three Lions kutenganishwa na wapigaji makasia kupitia dakika 30 za mazidadi.
Katika muda wa ziada kipindi cha kwanza Bellingham, alikumbana na mpira uliotemwa na kipa wa Norway ,Orjan Nyland akipangua tobwe la kiungo Morgan Rogers na kuuvurumiza kambirani.
Uingereza waliotwaa ubingwa mwaka 1966,walikaa ngumu na kujizatiti hadi kipenga cha mwisho na kufuzu kwa nusu fainali dhidi ya Argentina Jumatano ijayo.