Kaimu Katibu Mkuu wa ODM Catharine Omanyo ametetea uamuzi wa Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa, ORPP wa kumwondoa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kutoka wadhifa wa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Mwakilishi huyo wa Wanawake wa kaunti ya Busia amedai hatua hiyo ilitokana na kile alichosema ni ukiukaji wa maadili ya chama.
Omanyo pia ametoa wito kwa uongozi wa ODM kumuidhinisha rasmi kuwa Katibu Mkuu mpya.
Akizungumza katika hafla ya kuwawezesha wanawake iliyofanyika Maira, eneo bunge la Nambale, kaunti ya Busia, Omanyo alisema ana uwezo wa kutekeleza majukumu ya wadhifa huo na kusisitiza kuwa hataondoka ofisini hadi pale chama kitakapofanya uamuzi rasmi kuhusu nafasi hiyo.
Omanyo alidai kuwa hatua ya kumwondoa Sifuna imekuja wakati mwafaka, akimshutumu kwa kususia mikutano ya chama iliyoongozwa na kiongozi wa ODM, Dkt. Raila Odinga. Alisema viongozi wa chama wanapaswa kuunga mkono maamuzi ya uongozi na kuimarisha mshikamano ndani ya ODM.
Kauli zake zinawadia saa chache baada ya ORPP kumwondoa rasmi Sifuna kutoka kwenye orodha ya viongozi wa chama cha ODM kama Katibu Mkuu.
Ni hatua inayotazamiwa kukomesha miezi kadhaa ya mivutano kuhusu wadhifa wake.
Katika barua aliyotumiwa Sifuna kwa afisi yake bungeni jana Alhamisi, msajili wa vyama vya kisiasa alisema uamuzi huo ulifikiwa baada ya kudurusu nyaraka zilizowasilishwa na ODM.
Alisema aliweza kubaini kuwa Sifuna hakuwasilisha majibu kama inavyotakiwa chini ya Kifungu cha 47 cha Katiba.
Awali, Sifuna aliashiria kuwa ataelekea mahakamani kupinga kuvuliwa kwa wadhifa wa Katibu Mkuu wa ODM.
Seneta huyo wa Nairobi kwa sasa anaongoza vuguvugu la Linda Mwananchi na kunao wanaomtaka kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Taarifa hii imechangiwa na Sayyid Abdalla