Tamasha ya ‘I Am Hip Hop’ yarejea nchini Rwanda

Awamu ya mwaka huu itahusisha kanda na kukutanisha wasanii kutoka Rwanda, Uganda na Burundi.

Marion Bosire
2 Min Read
Riderman, Mwanamuziki wa Hip Hop, Rwanda.

Tamasha ya ‘I Am Hip Hop’ ya Kigali inarejea mwaka 2026 awamu hii ikihusisha kanda nzima na kukutanisha wasanii kutoka Rwanda, Uganda na Burundi.

Itakuwa wiki moja ya ushirikiano wa kisanii kabla ya tamasha ya siku mbili jijini Kigali.

Tamasha hiyo, inayoongozwa na Green Ferry Music na kufadhiliwa kwa pamoja na Institut français ya Paris na kuungwa mkono na Institut français du Rwanda, itafanyika Agosti 28 hadi 29 katika Taasisi ya Ufaransa nchini Rwanda.

Waandalizi wanasema ratiba ya tamasha hiyo itajumuisha maonyesho ya muziki, warsha na vipindi vya kurekodi studio vinavyolenga kuimarisha ujuzi wa wasanii katika sanaa za mijini Afrika Mashariki.

Zaidi ya wasanii 30 wanatarajiwa kushiriki vipengele vya rap, breakdance, graffiti na ubunifu wa mavazi ya mitaani.

Kabla ya tamasha ya hadhara, kutakuwa na vipindi vya ubunifu wa pamoja vitakavyojikita katika uandishi wa nyimbo, maonyesho ya jukwaani, sanaa za picha na ubunifu wa mavazi, huku washiriki wakishirikiana kuvuka mipaka ya taaluma na nchi zao.

Tamasha itahitimishwa kwa siku mbili za shughuli za wazi kwa umma zitakazojumuisha maonyesho ya rap mubashara, breakdance, graffiti, burudani za ma-DJ, maonesho ya mavazi ya mitaani pamoja na maduka ya muda.

Milango itafunguliwa kuanzia saa tisa alasiri hadi saa tano usiku katika siku zote mbili.

Tamasha ya I Am Hip Hop ilianzishwa mwaka 2017 kama mfululizo wa matamasha madogo ya muziki kabla ya kupanuliwa na kuwa tamasha kamili mwaka 2024.

Awamu ya mwaka 2026 inaashiria hatua mpya ya kuifanya tamasha hiyo kuwa ya kikanda.

Green Ferry Music imesema lengo la tamasha hiyo ni kujenga mtandao imara zaidi wa hip hop Afrika Mashariki huku ikiwapa wasanii chipukizi nafasi ya kujifunza, kushirikiana na kutumbuiza.

Share This Article