Waziri wa Fedha John Mbadi ameteua watu sita kuwa wanachama wa Bodi ya Mfuko wa Kitaifa wa Miundombinu (NIF).
Kwenye gazeti rasmi lililochapishwa Julai 8, Mbadi amesema sita hao watahudumu kwa kipindi cha miaka mitatu na kwamba uteuzi wao unaanza kutekelezwa mara moja.
Walioteuliwa kuwa wanachama wa bodi hiyo ni James Mworia Mwirigi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Centum Investment, Fahima Ali Ahmed Zein, Christopher Kibui Maranga na Latoya Ouna.
Wengine ni Lawrence Kibet na Mohammed Abdirahman Hassan.
Mnamo mwezi Machi mwaka huu, Rais Ruto alizindua NIF kwa lengo la kufadhili miradi mikubwa nchini kama vile barabara na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ruto alisema mfuko huo utaisaidia Kenya kufadhili miradi muhimu ya miundombinu na kupunguza utegemezi wa mikopo kutoka nje ya nchi.
Mradi wa kwanza mkubwa utakaofadhiliwa kupitia mfuko huo mpya utakuwa upanuzi wa JKIA unaotarajiwa kuanza wakati wowote.
Upanuzi wa uwanja huo umekabidhiwa kampuni ya China ya China Road and Bridge Corporation (CRBC).