Rais William Ruto leo Jumatano katika Ikulu ya Nairobi ametia saini kuwa sheria Mswada wa Mfuko wa Utajiri wa Kitaifa, 2026.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula miongoni mwa viongozi wengine.
“Mwezi Machi mwaka huu, Kenya ilibadili jinsi itakavyofadhili ustawi wake ili kujenga rasilimali za siku zijazo kupitia Mfuko wa Kitaifa wa Miundombinu,” alisema Rais Ruto wakati akihutubia hadhira baada kusaini mswada huo kuwa sheria.
“Leo, Kenya inabadili namna itakavyolinda utajiri wake. Leo, tunaweka katika sheria taasisi itakayohakikisha kuwa ustawi unaoletwa na rasilimali hizo unadumu kwa ajili ya vizazi vijavyo, Mfuko wa Utajiri wa Kitaifa.”
Ruto aliongeza kuwa huku Mfuko wa Kitaifa wa Miundombinu ukijenga rasilimali zinazoendeleza nchi hii, Mfuko wa Utajiri wa Kitaifa utalinda na kuongeza utajiri unaoletwa na rasilimali hizo.
Alirejelea Ajenda ya Mabadiliko kuanzia Chini hadi Juu (BETA) aliyosema imerejesha uthabiti, imani na kusaidia kuimarisha uchumi wa nchi wakati ikiweka misingi ya ukuaji endelevu na jumuishi.
“Huku kukiwa na misingi hiyo, sasa tunabadili jinsi Kenya inavyofadhili maendeleo, huku tukikusanya akiba za ndani na mtaji binafsi kujenga rasilimali za siku zijazo,” alisema Rais.
Aliashiria kuwa Mfuko wa Utajiri wa Kitaifa kwa sasa una thamani ya takriban shilingi trilioni 286 na unamiliki takriban asilimia 1.5 ya kampuni zote zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa duniani kote.
Aidha, alisema mfuko huo una uwekezaji wa zaidi ya kampuni 7,200 duniani kote.