Waathiriwa 157 wa maandamano kupokea milioni 225.4 kama fidia

Fedha hizo zinatolewa katika awamu ya pili ya malipo kwa waathiriwa. Shilingi milioni 448.7 zilitolewa kwa waathiriwa katika awamu ya kwanza.

Martin Mwanje
2 Min Read
Prof. Makau Mutua - Mwenyekiti wa Jopo la Fidia

Jumla ya waathiriwa 157 wa maandamano watakapokea shilingi milioni 225.5 kama fidia katika awamu ya pili ya ulipaji fedha hizo kwa waathiriwa. 

Hii itafanya fedha zilizotolewa kwa waathiriwa kuwa milioni 674.1 huku idadi ya waliofidiwa ikigonga 505 kufikia sasa.

Mwenyekiti wa Jopo la Fidia Prof. Makau Mutua amesema shilingi milioni 448.7 zilitolewa kwa waathiriwa katika awamu ya kwanza.

“Fedha hizi zinawakilisha asilimia 56 ya madai yote ya malipo yaliyopokelewa na kushughulikiwa. Jopo pia limepokea uthibitisho wa upokeaji wa fedha hizo kutoka kwa waathiriwa wengi,” alisema Prof. Mutua katika taarifa.

Ameongeza kuwa mchakato wa kuwalipa waathiriwa fidia utaendelea hadi waathiriwa wote waliotambuliwa watakapopokea fedha zao.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika awamu ya pili, jopo limeshughulikia madai 157 ya malipo yaliyopokelewa na kuthibitishwa.

Madai 57 yanahusisha vifo ambapo shilingi milioni tatu zitalipwa kama fidia kwa familia za kila mwathiriwa huku waathiriwa 19 wa majeraha makubwa wakilipwa shilingi milioni moja kila mmoja.

Waathiriwa 57 wa majeraha ya wastani watalipwa fidia ya shilingi laki 5, waathiriwa 18 wa majeraha madogo shilingi elfu 50 huku waathiriwa 6 wa dhuluma za kingono wakilipwa shilingi milioni moja.

Jopo hilo limesema limepokea madai ya malipo zaidi ya 400 tangu lilipotangaza mpango wa kuwalipa waathiriwa wa maandamano fidia huku madai zaidi yakizidi kupokelewa na kupigiwa msasa.

 

 

 

Share This Article