Serikali imeanzisha mpango wa kitaifa wa maandalizi kufuatia utabiri wa wataalamu wa hali ya hewa wa Kenya na kimataifa.
Utabiri huo unaonyesha uwezekano mkubwa wa kunyesha kwa mvua za El Niño katika msimu wa mvua fupi wa Oktoba hadi Desemba.
Naibu Rais Kithure Kindiki amesema serikali tayari imeanza maandalizi kulingana na Sheria ya Kitaifa ya Usimamizi wa Majanga, iliyotiwa saini kuwa sheria mwezi uliopita.
Akizungumza baada ya kuongoza kikao kilichokutanisha maafisa kutoka wizara, idara na mashirika mbalimbali serikalini katika makazi yake ya Karen, Nairobi, Kindiki alisema serikali imeanza kuchukua hatua mapema ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa inayotarajiwa.
Wataalamu wa hali ya hewa wameonya kuwa mvua ya El Niño inayotarajiwa inaweza kuathiri usalama wa chakula kutokana na uharibifu wa mazao, huku pia ikihatarisha afya na usalama wa wananchi.
Aidha, mvua hiyo inaweza kuharibu miundombinu na kuvuruga usafiri na shughuli za ugavi wa bidhaa nchini.
Katika kikao hicho, Naibu Rais alipokea taarifa kuhusu hali ya Kenya kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kindiki alisema taasisi husika ziliwasilisha taarifa kuhusu hatua za ufuatiliaji na mwitikio, ambazo zitaimarishwa zaidi ili kuhakikisha nchi inalindwa dhidi ya hatari yoyote ya kiafya inayoweza kuvuka mipaka.
Serikali imeahidi kuendelea kufuatilia mwenendo wa utabiri wa hali ya hewa pamoja na hali ya afya ya umma katika ukanda huu huku ikiimarisha zaidi hatua za maandalizi ili kuwalinda Wakenya