Ujenzi wa reli ya SGR kati ya Naivasha-Kisumu-Malaba waanza

Ujenzi huo unafanywa na serikali ya Kenya kupitia Shirika la Reli la Kenya Railways, KR, na uzinduzi wake ulifanywa na Rais William Ruto mwezi Machi mwaka huu.  

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto wakati wa uzinduzi wa reli ya SGR mwezi Machi, 2026

Ujenzi uliosuburiwa kwa hamu wa reli ya SGR kati ya Naivasha-Kisumu-Malaba unaanza leo Jumatano miezi mitatu baada ya mradu huo kuzinduliwa rasmi na Rais William Ruto. 

Ujenzi huo unafanywa na serikali ya Kenya kupitia Shirika la Reli la Kenya Railways, KR.

Gavana wa Narok Patrick Ole Ntutu na Mkurugenzi Mkuu wa KR Pihilip Mainga ni miongoni mwa watakaohudhuria hafla ya kung’oa nanga kwa ujenzi wa reli hiyo katika Chuo cha Mafunzo ya Walimu mjini Narok.

“Mradi huu wa mabadiliko ya miundombinu unaashiria hatua kubwa katika kuimarisha uunganishaji wa usafiri, kuboresha biashara ya kikanda na kufungua fursa za kiuchumi eneo lote la Magharibi mwa Kenya na eneo pana la Afrika Mashariki,” ilisema KR kwenye taarifa.

“Mradi huu unatarajiwa kuboresha kwa kiwango kikubwa usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo, kuchochea ukuaji uchumi na kuongeza kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwenye ushoroba huo.”

Ujenzi huo unaanza baada ya Rais William Ruto Machi 19 kuzindua awamu ya 2B ya ujenzi wa reli ya SGR katika hafla iliyofanyika katika kaunti ya Narok.

Awamu ya 2B inahusisha ujenzi wa SGR kutoka mjini Naivasha hadi Kisumu.

Kisha siku mbili baadaye, Ruto pamoja na Rais wa Uganda Yoweri Museveni walizindua awamu ya 2C inayohusisha ujenzi wa reli hiyo kutoka mji wa Kisumu hadi mji wa mpakani wa Malaba katika kaunti ya Busia.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Ruto alisema kuna umuhimu wa kujenga reli hiyo hadi kufika Kisumu, Busia na kisha nchi zingine za Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC ili kuhakikisha manufaa yake yanadhihirika wazi.

Kulingana naye, mradi huo utasaidia mno kupunguza gharama ya kufanya biashara na usafiri, na usafirishaji wa bidhaa kati ya nchi za Afrika Mashariki.

Reli hiyo ya umbali wa kilomita 107, itaunganishwa na ile ya kutoka Mombasa ikijumuisha umbali wa kilomita 1,000 kutoka Mombasa hadi Malaba na kuingia nchini Uganda.

 

Share This Article