Polisi wanachunguza kutoweka kwa mwanaharakati Davis Lichuma

Tom Mathinji
1 Min Read
Polisi wanachunguza madai ya kutoweka kwa mwanaharakati Davis Lichuma.

Huduma ya Taifa ya Polisi, imesema imepokea habari kuhusu kutoweka kwa Davis Lichuma, ambaye ni mwanaharakati anayedaiwa kutoweka wakati wa maandamano ya Juni 25, Jijini Nairobi.

Kupitia kwa taarifa Jumapili, huduma hiyo ilisema habari kuhusu kutoweka kwa mwanaharakati huyo imerekodiwa katika kituo cha polisi cha Central Jijini Nairobi.

Wakati huo huo Polisi wamesema wanachunguza habari za  kutoweka kwa lazima na mateso, zinazoenezwa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ikitoa wito kwa yeyote aliye na habari kuhusu madai kama hayo kupiga ripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu.

“Tumepokea habari za kutoweka kwa mtu aliyetambuliwa kama Davis Lichuma, zilizoripotiwa katika kituo cha polisi cha Central Jijini Nairobi. Tunahakikisha kuwa ripoti zote zitachunguzwa vilivyo, kwa utalaam, bila mapendeleo, kwa haraka na kuamabatana na sheria,” ilisema taarifa ya Huduma ya Taifa ya Polisi.

“Tunatoa wito kwa yeyote aliye na habari kuhusu madai hayo ya kutoweka kwa lazima, mateso au ukiukaji wa haki za binadamu, kuripoti mara moja katika kituo cha polisi kilicho karibu,” iliogeza taarifa hiyo.

Aidha, huduma hiyo ilikariri kujitolea kwake kutekeleza utaalam, kuheshimu haki za binadamu na kuzingatia katiba ya Kenya na sheria zote zilizopo, ikisema imejitolea kuwalinda Wakenya wote, wakazi na wageni.

TAGGED:
Share This Article