Croatia waliwazabua Black Stars kutoka Ghana mabao 2-1 ,katika mechi ya mwisho ya kundi L ya Kombe la Dunia, iliyosakatwa ugani Philadelphia,Marekani, Jumamosi usiku.
Petar Sucic na Nikola Vlasic, walipachika magoli ya Croatia kunako dakika za 31 na 78 mtawalia, naye Derrick Luckassen, akakomboa kwa Ghana.
Three Lions ya Uingereza waliikomoa Panama magoli 2-0, katika mechi nyingine iliyopigwa sanjari kiwarani Metlife.
Uingereza walihemeshwa kipindi cha kwanza huku wakibanwa na kutoka sare tasa dakika 45 za kwanza.
Waingereza waliongeza shinikizo kipindi cha pili na bahati mtende ikasimama baada ya Jude Bellingham,kuunganisha pasi yake Bukayo Saka na kufunga goli la kwanza dakika ya 62.

Dakika tano baadaye nahodha Harry Kane, aliwanyanyua mashabiki wa Three Lions,akiunganisha pasi maridhawa kutoka kwa Bellingham na kusajili bao la pili.
Uingereza waliongoza kundi L kwa pointi of 7,moja zaidi ya Croatia waliochukua nafasi ya pili, wote wakiambatana kuelekea raundi ya pili ,wakati Ghana walikifuzu kwa kumaliza katika mojawapo wa nafasi za tatu bora.
Panama iliyaaga ilitimuliwa kwenye kinyang’anyiro cha mwaka huu kama timu pekee ambayo haikufunga goli baada ya mechi tatu walizopiga.