Shirika la Utangazaji Nchini Kenya (KBC) na Shirika la Hubei Media Group la China zimetia saini mkataba wa ushirikiano wa mawasiliano, unaolenga kuimarisha ubadilishanaji wa habari, utayarishaji wa vipindi, ubadilishanaji wa teknolojia na kuimarisha uwezo kati ya mashirika hayo mawili.
Makubaliano hayo yalitiwa saini wakati wa sherehe ya ufunguzi wa wiki ya Seeing China Hubei Media 2026, iliyoandaliwa jijini Nairobi.
Ni hatua inayofungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa vyombo vya habari kati ya Kenya na China.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa KBC Agnes Kalekye alisema ushirikiano huo unaashiria ukurasa mpya katika kuimarisha uhusiano baina ya watu kupitia simulizi za hadithi.
Kalekye alidokeza kuwa shirika la KBC lina jukumu muhimu la kuelimisha, kufahamisha na kuungaisha jamii, akiongeza kuwa ushirikiano huo utawezesha nchi hizo mbili kudumisha tamaduni zao, huku zikibuni fursa kwa wanahabari na wabunifu.
“KBC itakuwa mshirika. Tutaboresha maktba zetu kuwa za kidijitali….tutabuni majukwaa ambapo wasanii wa Kenya na China watajifunza mengi na kukua pamoja,” alisema Kalekye.