Hatima ya wawakilishi wa Afrika Senegal katika makala ya mwaka huu ya Kombe la Dunia itabainika leo Ijumaa usiku watakapomenyana na Iraq katika mchuano wa mwisho wa kundi I uwanjani Toronto, Canada.
Simba wa Teranga ambao hawana alama baada ya kupoteza mechi mbili za ufunguzi hawana budi kuwashinda Iraq kwa idadi kubwa ya mabao ili kuwa miongoni mwa timu nane bora zitakazofuzu kwa hatua ya 32 bora.
Ufaransa watakabiliana na Norway katika mchuano mwingine kuanzia saa nne katika uwanja wa Boston, timu zote zikiongoza kwa alama sita baada ya kushinda mechi mbili za ufunguzi.
Saa tisa alfajiri, Cape Verde watapimana ubabe na Saudi Arabia katika kundi H uwanjani Boston, Papa wa visiwani Cape Verde wakihitaji ushindi ili kujihakikishia nafasi kwa raundi ya 32 bora.
Aidha, Cape Verde watafuzu endapo watapata sare.
Viongozi wa kundi H Uhispania watachuana na Uruguay katika uchanjaa wa Guadalajara pia.
Misri watalenga ushindi ili kuongoza kundi G watakaposhikana mashati na Iran katika uga wa Seattle nchini Marekani kuanzia saa kumi na mbili asubuhi Jumamosi.
Ubelgiji watashuka uwanjani BC Vancouver, Canada pia saa kumi na mbili asubuhi dhidi ya New Zealand, The Red Devils wakihitaji ushindi ili kufuzu kwa hatua ya 16 bora.