Wanasiasa wazuiwa kuweka majina na picha zao kwenye miradi ya umma

Wabunge hasa wana hulka ya kuandika majina na kuweka picha zao kwenye miradi iliyofadhiliwa na pesa za umma kama vile NG-CDF.

Martin Mwanje
3 Min Read

Wanasiasa wamepigwa marufuku kuandika majina au kuweka picha zao kwenye miradi inayofadhiliwa na pesa za umma. 

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imetaja hatua hiyo kuwa inayokiuka sheria na inayopaswa kukoma mara moja.

“Nadhari ya Tume imeelekezwa kwa mwenendo unaoibukia wa kuandika majina na kuweka picha au nembo ya watu mahususi, vyama vya kisiasa, au viongozi kwenye miradi na mipango ya umma. Ripoti mbalimbali zilizopokelewa na Tume zinaashiria kuwa viongozi fulani wa kisiasa wakati wote huweka majina au picha zao kwenye miradi na mipango iliyofadhiliwa na fedha za umma,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa EACC, Abdi Mohamud kwenye taarifa.

“Ingawa utambuzi wa huduma ya umma ni muhimu, kuweka majina au picha kwenye miradi na mipango iliyofadhiliwa na fedha za umma ni utumiaji mbaya wa afisi, utumiaji mbaya wa rasilimali za umma na ukiukaji wa maadili kinyume cha Vifungu vya 10, 73, na 75, 201(d) vya Katiba ya Kenya, 2010, Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma, 2012 na Sheria ya Uongozi na Maadili, 2022.”

Kutokana na hilo, EACC sasa imewaka maafisa wa serikali na umma, kuepuka kutumia rasilimali za umma kuendeleza maslahi yao ya kibinafsi au ya kisiasa.

Taasisi husika za umma pia zimetakiwa kuhakikisha majina au picha za watu binafsi vinaondolewa mara moja kwenye miradi iliyofadhiliwa na fedha za umma.

“Taasisi husika za umma zinazotekeleza agizo hilo zinapaswa kuhakikisha kuwa pale ambapo utambuzi ni muhimu, unapaswa kutambua tu taasisi ya umma husika na kuonyesha bayana ikiwa mradi au mpango huo unafadhiliwa na serikali kuu au ya kaunti, bila kuweka majina au picha ya mtu binafsi,” iliagiza EACC kwenye taarifa hiyo.

Tume hiyo imesema itafuatilia utekelezaji wa agizo hilo na watakaolikiuka wanaweza wakachukuliwa hatua za kisheria.

Wanasiasa hasa wabunge wana hulka ya kuandika au kuweka majina yao kwenye miradi inayofadhiliwa na fedha za umma, hasa ile inayofadhiliwa na Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji wa Maeneo Bunge, NG-CDF kama vile madarasa.

Huku uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ukikaribia, hulka hiyo ilielekea kupamba moto huku wabunge wakijitafutia umaarufu katika jitihada zao za kuchaguliwa tena kuhudumu kwa muhula mwingine.

Haijulikani ikiwa agizo hilo litazingatiwa kikamilifu.

 

 

Share This Article