Ruto aainisha mikakati ya kuongeza uzalishaji wa kahawa nchini

Martin Mwanje
3 Min Read
Rais William Ruto akiwa na viongozi wengine wakati wa uzinduzi wa mpango wa kufufua sekta ya kahawa katika eneo Kianyaga, kaunti ya Kirinyaga

Rais William Ruto ameelezea mikakati mbalimbali inayopangwa kutekelezwa na serikali yake ili kuongeza uzalishaji wa kahawa nchini.

Kipaumbele kwenye mikakati hiyo inajumuisha kupanua maeneo ya kilimo cha zao hilo kwa kuyajumuisha yale yenye uwezo mkubwa kama vile eneo la Magharibi, Nyanza, Bonde la Ufaa na maeneo mengine yanayofaa.

“Kupitia uzalishaji mkubwa na upanuzi wa kilimo, tutaongeza eneo la kahawa kutoka hekta 110,000 hadi hekta 150,000 ndani ya miaka miwili ijayo,” alisema Ruto wakati akizindua mpango wa ufufuzi wa sekta ya kahawa nchini katika eneo la Kianyaga, kaunti ya Kirinyaga leo Jumatatu.

“Kadri uzalishaji unavyoongezeka, lazima pia tuboreshe uwezo wa utayarishaji zao hilo; yaani processing. Viwanda vingi vya ushirika bado vinatumia mashine za zamani na mifumo isiyofaa. Tutatoa mashine za kisasa na kuboresha ukaushaji na uhifadhi wa kahawa ili tuweze kuuza kahawa bora zaidi katika masoko ya kimataifa: yaani premium coffee.”

Rais Ruto pia alisisitiza umuhimu wa wakulima kujiunga na vyama vya ushirika ili kusaidia kupiga jeki juhudi za kuongeza uzalishaji wa kahawa nchini.

Alisema kwa kujiunga na vyama hivyo, wakulima wataweza kuuza zao hilo kwa pamoja, kuboresha ubora, kupata pembejeo kwa bei nafuu, kutayarisha mazao yao pamoja, na kujitetea kwa pamoja huku vyama vya ushirika sasa vikiweza kuuza kahawa moja kwa moja kwa wanunuzi duniani kupitia Soko la Kahawa la Nairobi yaani Nairobi Coffee Exchange.

“Pia tunarekebisha mfumo wa malipo. Angalau asilimia 80 ya mapato ya mauzo ya kahawa lazima yaende moja kwa moja kwa mkulima, huku watoa huduma wakigawana asilimia 20 iliyobaki,” aliongeza Ruto.

“Aidha, kupitia Mfumo wa Malipo ya Moja kwa Moja, wakulima sasa watapokea malipo ndani ya siku tano baada ya mauzo. Hakutakuwa tena na kusubiri kwa wiki, miezi au misimu mizima. Kulipwa kwa wakati si hisani kwa mkulima; ni haki yake.”

Alielezea imani kuwa teknolojia pia itasaidia kulinda mapato ya wakulima kupitia rekodi za kidijitali zilizo wazi ambazo zitawazuia madalali na walanguzi ambao wamezeoa kula wasikopanda. Kulingana naye, hatua hii pia itaimarishwa kupitia mswada wa Vyama vya Ushirika ambao tayari umewasilishwa bungeni.

Kenya kwa sasa huzalisha takriban tani 50,000 za kahawa kila mwaka huku nchi hiyo ikinuia kuongeza uzalishaji huo mara tatu hadi tani 150,000 kufikia mwaka 2028.

 

Share This Article