Ruto azindua mpango wa kufufua sekta ya kahawa nchini

Kenya kwa sasa huzalisha takriban tani 50,000 za kahawa kila mwaka.

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto

Rais William Ruto leo Jumatatu amezindua mpango wa kufufua sekta ya kahawa nchini kupitia kwa vyama vya ushirika. 

Lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha mkulima anajipata mapato zaidi kupitia kilimo cha zao hilo.

Kenya kwa sasa huzalisha takriban tani 50,000 za kahawa kila mwaka.

“Lengo letu ni kuongeza uzalishaji huo mara tatu hadi tani 150,000 kufikia mwaka 2028,” alisema Rais Ruto wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango huo iliyofanyika katika eneo la Kianyaga, kaunti ya Kirinyaga leo Jumatatu na kuhudhuriwa na Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki.

“Tutafanikisha hili kwa kuongeza maeneo ya kilimo na kuboresha uzalishaji kwa kiwango kikubwa. Kwa sasa mti mmoja wa kahawa nchini Kenya huzalisha takriban kilo mbili. Kupitia miche bora, mbolea ya kutosha, ushauri wa kitaalamu kwa wakulima, na mbinu za kisasa za kilimo, tutaongeza uzalishaji hadi angalau kilo sita kwa kila mti.”

Ruto alisema ni kwa misingi hiyo ndiposa serikali yake inawagawia wakulima mamilioni ya miche bora na kuahidi kuwasaidia katika kila hatua kwa lengo la kuhakikisha miche hiyo inamea, kukomaa na kuwa chanzo chao cha mapato yao.

“Pia tunapunguza gharama za uzalishaji. Tumeipunguza bei ya mbolea kutoka shilingi 7,500 hadi shilingi 2,500 kwa gunia, na tutaendelea kutoa mbolea zaidi, dawa za kuzuia magonjwa na wadudu, pamoja na vifaa vya kisasa vya kilimo,” aliongeza Ruto katika hafla ambayo pia ilihudhuriwa na Gavana wa Kirinyanga Anne Waiguru.

Miongoni mwa mambo mengine, kiongozi wa nchi aliahidi kupanua kilimo cha kahawa katika maeneo mengine yenye uwezo mkubwa kama vile Magharibi mwa nchi, Bonde la Ufa na Nyanza, na kuongeza eneo la kahawa kutoka hekta 110,000 hadi hekta 150,000 ndani ya kipindi cha miaka miwili ijayo.

 

Share This Article