Papa wa Sawamati ukipenda Blue Sharks kutoka Cape Verde waliitoa Uruguay jasho puani, baada ya kulazimisha sare ya mabao 2 katika mtanange wa kundi H uliosakatwa Jumatatu alfajiri uwanjani Miami, Marekani.
Cape Verde wanaoshiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza walichukua uongozi wa mechi hiyo dakika ya 21 kupitia kwa Kevin Lenini huku mabingwa mara mbili Uruguay wakisawazisha dakika ya 42 ya kipindi cha kwanza kupitia kwa Maximiliano Araujo.
Agustin Canobbio aliwaweka Uruguay uongizini dakika za mwisho za kipindi cha kwanza.
Cape verde walidhihirisha mchezo wa hali ya juu wa kujihami na mashambulizi ya uhakika yaliyozaa matunda baada ya Helio Varela kukomboa bao la dakika ya 61.
Licha ya mashambulizi tele kutoka kwa Uruguay, Papa wa visiwa vya Cape Verde walionekana kutotetereka na kuzoa sare ya pili baada ya kuwashika mateka mabingwa wa Ulaya, Uhispania katika mechi ya ufunguzi.
Uhispania walioikomoa Saudi Arabia mabao 4-0, wanaongoza kundi hilo kwa alama 4 wakifuatwa na Uruguay na Cape Verde kwa pointi 2 kila moja wakati Saudia ikishika mkia kwa alama 1.