Mbappe afumua Simba wa Teranga

Senegal ni sharti washinde mechi ya pili dhidi ya Norway Juni 23 ili kuwa na matumaini ya kufuzu kwa raundi ya 32 bora.

Dismas Otuke
2 Min Read

Kyllian Mbappe alicheka na nyavu mara mbili kunako kipindi cha pili na kuwasaidia mabingwa mara mbili -Ufaransa, kuwagaragaza Senegal magoli 3-1 kwenye mechi ya kundi I iliyosakatwa uwanjani New York, New Jersey nchini Marekani Jumanne usiku.

Baada ya timu zote kutoshana nguvu ya kutofungana katika kipindi cha kwanza, makocha Didier Deschamp wa Ufaransa na mwenzake wa Senegal Pape Thiaw, walirejea kipindi cha pili na mbinu tofauti ya kupiga mashambulizi.

Mbappe alifungua ukurasa wa goli katika dakika ya 66, kabla ya Bradley Barcola kutanua uongozi kwa goli la dakika ya 82.

Ibrahim Mbaye alikomboa moja kwa Senegal kunako dakika ya 95 kabla ya Mbappe kupachika bao la tatu dakika ya 96.

Mbappe aliweka rekodi mpya ya kuwa mfungaji bora wa Ufaransa akiwa na magoli 58, moja zaidi ya Olivier Giroud.

Aidha, Mbappe huenda avunje rekodi ya Miroslave Klose ya kuwa mfungaji bora katika historia ya Kombe la Dunia ya magoli 16, Mfaransa huyo akiwa tayari amefunga 14 baada ya mechi ya jana.

Senegal ni sharti washinde mechi ya pili dhidi ya Norway Juni 23 ili kuwa na matumaini ya kufuzu kwa raundi ya 32 bora.

Upande wa pili wa sarafu, The Blues wanahitaji ushindi dhidi ya Iraq katika mechi ya pili Juni 23 ili kujikatia tiketi ya raundi ya pili.

Share This Article