Ivory Coast imekuwa timu ya kwanza ya Afrika kusajili ushindi katika Kombe la Dunia mwaka huu, baada ya Amad Diallo kupachika bao la dakika za mwisho katika mechi ya kundi E iliyopigwa Jumapili usiku mjini Philadelphia nchini Marekani.
Timu zote zilidhihirisha mchezo wa hali ya juu huku zikitoka sare tasa katika dakika 45 za kwanza.
Kipindi cha pili pia hali haikuwa tofauti na kilikuwa kikielekea sare pia kabla ya Wifred Singo kumpakulia pasi Diallo kunako dakika ya 90 naye bila kusita akatikisa nyavu.
Ushindi huo unawafanya Tembo wa Ivory Coast kuwa timu ya kwanza ya Afrika kushinda mechi katika fainali za mwaka huu.
Ujerumani wanaongoza kundi E kwa pointi 3 sawa na Ivory Coast huku Ecuador na Curacao wakishika mkia kwa pamoja pasi na alama.