Serikali ya Malawi imesema hivi karibuni itaanza kuwarejesha nyumbani raia wake walio Afrika Kusini kufuatia visa vya ghasia dhidi ya raia wa kigeni vinavyoshuhudiwa nchini humo.
Kupitia kwa taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imesema imekuwa ikifuatilia taarifa kuhusu mashambulizi dhidi ya wahamiaji wa kiafrika, na imeshauriana na mamlaka ya Afrika Kusini kupitia mifumo ya kidiplomasia.
“Kupitia ubalozi wa Pretoria na afisi ya ujumbe ya Johannesburg, wizara hiyo imeshauriana na viongozi wa makundi ya raia wa Malawi Afrika Kusini ili kukadiria hali na kuwasaidia wale walioathiriwa,” ilisema taarifa hiyo.
Aidha, wizara hiyo ilidokeza kuwa itawasaidia tu raia wa Malawi ambao wanataka kurejea nyumbani kwa hiari.
Hata hivyo, wizara hiyo imewataka raia wake nchini Afrika Kusini kuchukua kujihadhari na wanaojisingia kuwa wawakilishi wa serikali, huku ikisisitiza kuwa haijamhusisha mtu yeote au taasisi kuwarejesha nyumbani raia hao.
Mashambulizi hayo yamesalia kuwa kero nchini Afrika Kusini, ambako raia wa kigeni wamekuwa wakilaumiwa kwa kusambaratisha uchumi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ajira.
Serikali ya Afrika kusini imeshutumu mashambulizi hayo na kuahidi kuwachukulia hatua waliohusika nayo.