Uchumi wa Kanda ya Afrika Mashariki unatarajiwa kuendelea kuimarika kwa kasi zaidi barani Afrika, katika kipindi cha mwaka 2026/2027, licha ya changamoto zinazoendelea kushuhudiwa.
Kwenye ripoti ya kiuchumi iliyotolewa na Benki ya Maendeleo ya Bara Afrika (AfDB), uchumi wa kanda ya Afrika Mashariki utapungua hadi asilimia 5.9 mwaka 2026 kutoka asilimia 6.6 mwaka 2025, lakini unatarajiwa kuimarika hadi asilimia 6.4 mwaka 2027.
Aidha ripoti hiyo ilidokeza kuwa uchumi wa Afrika kwa jumla unatarajiwa kuimarika hadi asilimia 4.4 mwaka 2027 kutoka asilimia 4.2 mwaka 2026.
Katika mwaka 2027 kanda ya Afrika Mashariki inatarajiwa kuwa kifua mbele kuliko maeneo mengine, huku kanda ya Kaskazini mwa Afrika ikitarajiwa kuwa na ukuaji wa asilimia 4.2, Afrika Magharibi asilimia 4.5, Afrika Kati asilimia 4.1, na Afrika Kusini asilimia 2.7.
Benki hiyo ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ilitoa ripoti hiyo kwenye mkutano wake wa mwaka ulioandaliwa Jijini Brazzaville, katika jamhuri ya Congo.