Jumla ya wanafunzi 8 wanazuiliwa kuhusiana na mkasa wa moto uliosababisha vifo vya wanafunzi 16 katika shule ya Utumishi Girls Academy, mjini Gilgil katika kaunti ya Kakamega.
Wanafunzi wengine 79 walijeruhiwa na 72 kutibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani huku saba wakilazwa hospitalini.
Kwenye taarifa, Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI inasema uchunguzi kubaini chanzo cha moto huo unaendelea ukihusisha wapelelezi wabobezi kuhusiana na suala hilo.
“Uchunguzi wa awali umetambua wanafunzi 8 kama watu wanaoshukiwa kuhusika katika upangaji na utekelezaji wa shambulizi la uchomaji wa bweni hilo kimakusudi. Wanane hao wamekamatwa na kwa sasa wanazuiliwa na polisi,” alisema Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin kupitia kwa taarifa iliyotumwa na afisa wa mawasiliano wa idara hiyo, John Marete.
Amin anasema waplelezi wanaendelea kuandikisha taarifa na kuchambua ushahidi wote uliopo ili kufahamu matukio kabla ya kutokea kwa mkasa huo na kubaini dhamira yake.
Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen amewahakikishia Wakenya kuwa serikali itafanya kila iwezalo kuwawajibisha wahusika wa mkasa huo.
Mipango ya kufanya uchunguzi wa vinasaba (DNA) inaendelea ili kutambua miili ya wanafunzi walioteketea.
Mwanapatholojia Mkuu wa Serikali Dkt. Titus Ngulungu amesema shughuli ya kutoa miili 16 katika vifusi vya bweni hilo imekamilika.
Miili hiyo imepelekwa katika makafani ya Hospitali ya Naivasha kwa upasuaji na tathmini zaidi.
Aliongeza kuwa mingi ya miili hiyo iliteketea hadi kiwango cha kutoweza kutambulika.