Uchunguzi wa DNA kuandaliwa kubaini miili ya wanafunzi walioteketea Utumishi Academy

Mingi ya miili hiyo iliteketea hadi kiwango cha kutotambulika. Wanafunzi 16 waliangamia kwenye mkasa wa moto uliotokea shuleni hapo jana Alhamisi.

Dismas Otuke
1 Min Read

Uchunguzi wa vinasaba (DNA) utafanyika ili kutambua miili ya wanafunzi walioteketea katika shule ya upili ya wasichana ya Utumishi Academy mapema jana Alhamisi mjini Gilgil katika kaunti ya Nakuru.

Mwanapatholojia Mkuu wa Serikali Dkt. Titus Ngulungu alisema Alhamisi usiku kuwa shughuli ya kutoa miili 16 katika vifusi vya bweni hilo imekamilika.

Miili hiyo imepelekwa katika makafani ya Hospitali ya Naivasha kwa upasuaji na tathmini zaidi.

Aliongeza kuwa mingi ya miili hiyo iliteketea kiwango cha kutotambulika.

Wanafunzi wengine 79 walijeruhiwa wakati wa mkasa huo huku 72 wakitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Saba walilazwa hospitalini kwa matibabu zaidi baada ya kupata majeraha mabaya.

Baadhi ya wanafunzi wamesafirishwa hadi Hospitali ya Kitaifa ya Rufaa ya Kenyatta, KNH kwa matibabu maalum.

Uchunguzi kubaini chanzo cha moto kwenye shule ya Utumishi Girls Academy unaendelea.

Mamlaka zimeahidi kumchukulia hatua kali yeyote anayeweza kuwa alihusika katika kusababisha mkasa huo.

Share This Article