Wanafunzi 16 wamefariki kutokana na mkasa wa moto uliotokea mapema leo Alhamisi katika Shule ya Wasichana ya Sekondari ya Juu ya Utumishi Girls Academy mjini Gilgil, kaunti ya Nakuru.
Waziri wa Elimu Julius Ogamba amesema wanafunzi wengine 79 walijeruhiwa wakati wa mkasa huo uliotokea saa 6:45 usiku wa kuamkia leo.
Wanafunzi 7 bado wamelazwa hospitalini wakipokea matibabu.
Wanafunzi 71 walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani. Mwanafunzi mmoja kati ya 79 hao alichukuliwa na mzazi.
Akiwahutubia wanahabari leo Alhamisi kutoka shuleni hapo, Ogamba alisema wanafunzi 808 walikuwa shuleni wakati wa mkasa huo.
Shule hiyo iliyoanzishwa na mnamo mwaka 2020 ina jumla ya wanafunzi 815 na wanafunzi saba walikuwa wameenda nyumbani kwa sababu mbalimbali.
Waziri Ogamba amesema mchakato wa kutambua miili ya wanafunzi waliofariki unaendelea.
Kwa upande wake, Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen ametoa wito wa utulivu wakati uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha mkasa huo.
Shirika la Msalaba Mwekundu na asasi zingine za serikali zimetenga vituo kadhaa karibu na shule hiyo kutoa huduma ya kwanza na ushauri nasaha kwa familia za wanafunzi walioathiriwa.