Ousmane Sonko: Waziri Mkuu aliyetimuliwa, achaguliwa kuwa Spika

radiotaifa
2 Min Read
Ousmane Sonko aliyechaguliwa kuwa Spika

Ousmane Sonko mwenye umri wa miaka 51 amechaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Taifa la Senegal leo Jumanne, akimrithi El Malick Ndiaye ambaye alijiuzulu Jumapili.

Sonko alikuwa Waziri Mkuu kuanzia Aprili 2024 hadi Mei 2026, lakini alifutwa kazi Ijumaa iliyopita na Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, na nafasi yake kuchukuliwa na Ahmadou Al Aminou Mohamed Lo mwenye umri wa miaka 60, aliyekuwa afisa wa Benki ya Afrika Magharibi.

Spika mpya wa Bunge la Senegal alisema kuhusu mvutano uliopo kati yake na Rais Bassirou Diomaye Faye: “Kinachowekwa mezani ni uhusiano kati ya maadili na siasa.” Aliongeza kuwa hatatumia nafasi yake mpya “kupambana na mtu yeyote, na atahakikisha bunge linafanya kazi kwa uwajibikaji kwa maslahi ya wananchi.”

Sonko pia alisema kuwa kufutwa kwake kazi hakumaanishi mwisho wa maisha yake ya kisiasa.

Wakati akipongeza kazi ya Waziri Mkuu mpya Ahmadou Al Aminou Lô, ambaye hapo awali alikuwa Waziri katika Ofisi ya Rais anayehusika na ufuatiliaji, uongozi na tathmini ya ajenda ya mabadiliko ya Taifa ya Senegal 2050, Sonko alitaja kuwepo kwa “tofauti fulani” kuhusu masuala ya fedha na madeni.

“Chama chetu hakikuhusishwa katika uamuzi huu,” alisema kuhusu uteuzi wa mkuu mpya wa serikali. “Huwezi kuwa na Pastef bila Pastef,” alitangaza. “Pastef bado iko wazi kwa mazungumzo ya kuwajibika yanayoweka pembeni ubinafsi ili kukamilisha muhula huu katika mazingira bora zaidi.”

Waziri Mkuu huyo wa zamani, ambaye pia ni kiongozi mwenye ushawishi mkubwa wa chama cha PASTEF, aliongoza orodha ya wabunge ya chama chake katika uchaguzi wa wabunge wa Novemba 2024. Ingawa alichaguliwa kuwa mbunge, aliacha majukumu yake ya kibunge ili kuendelea kuhudumu kama Waziri Mkuu.

Mwezi uliopita, wabunge waliidhinisha kwa wingi mabadiliko ya sheria ya uchaguzi ambayo yanaweza kufungua njia kwa Sonko kugombea urais mwaka 2029.

Taarifa ya BBC

Share This Article