Mageuzi yaliyoanzishwa na serikali katika sekta ya sukari miaka minne iliyopita yameanza kuzaa matunda.
Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki anasema mageuzi hayo yameboresha usimamizi, kufufua viwanda vilivyokuwa vimefunga na hivyo kuhakikisha malipo yanatolewa kwa wakulima na wafanyakazi kwa wakati.
“Mashamba ya kilimo cha miwa yameongezeka kwa hekari 200,ooo, huku uzalishaji na mapato ya wakulima yakiongezeka kutokana na ruzuku za mbolea,” amesema Naibu Rais.
“Mustakabali wa sekta ya sukari ni ule ambao utazalisha siyo tu sukari, lakini pia kemikali aina ya ethanol, mafuta ya usafiri wa anga, nishati mbadala, kemikali za bio na bidhaa zingine za viwanda za thamani ya juu.”

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Kongamano la Kimataifa la 68 la Sukari huko Diani, kaunti ya Kwale, Prof. Kindiki alisema nchi hii inaunga mkono mfumo wa biashara ya kimataifa uliojikita kwenye sheria katika bidhaa za sukari na bidhaa zingine za kilimo.
Amesema mfumo huo ni muhimu katika kuhamasisha maslahi ya nchi wazalishaji na watumiaji.